Please Wait
11500
Wakristo walipokuwa wakiishi katika zama ambazo Isa (a.s) alikuwa tayari ameshapaishwa mbinguni na Mola wake, jukumu la kulingania dini lilishikwa na mitume pamoja na wafuasi wake (Hawariyyuun), waliokuwepo kwa ajili yake ndani ya zama hizo, na licha ya mitume na wafuasi hao kupata adhabu mbali mbali pale walipokuwa wakiitangaza dni hiyo, lakini wao hawakuiweka nyuma dini hiyo wala kuachana nayo.
Lakini baada ya kupita muda si mrefu alitokea mtu mmoja ajulikanye kwa jina la “Paul”, naye ndiye mfinyanzi mkuu wa mfumo wa Ukristo uliopo katika zama zetu za hivi sasa, yeye basi alikuja na kukivaa kilemba cha uongozi wa Ukristo ndani ya zama hizo. Paul mwanzoni mwa maisha yake alikuwa ni Myahudi aliyewatesa na kuwaudhi sana Wakristo, na baadae akaingia katika dini ya Kikristo, hatimae yeye aliweza kukubalika vizuri sana mbele ya Wakristo. Paul katika utendaji wake alijiweka kama ni mtume (mjumbe) wa Isa (a.s) na akawa anatembea katika vitongoji mbali mbali akiutangaza Ukristo huku akiusongomanisha na kuuposha hatua baada ya hatua.
Katika kipindi cha miaka iliofutia baadae, kipindi ambacho kilijulikana kwa jina la kipindi cha miaka ya kati na kati (middle ages), wanachuoni wa Kikristo walijitahidi sana kutaka kuirekebisha ile misongomano ya itikadi iliyopandikizwa ndani ya Ukristo wa kileo kutoka kwa Paul, wao walijitahidi kutoa tafsiri na kuzipa picha nzuri zile itikadi zisizoendana na akili, walifanya hivyo ili kuzifanya itikadi hizo zikubaliane na akili za wanaadamu wailo salama kiakili. Ingawaje wao walipoteza muda mwinga katika juhudi za kutafuta suluhu, lakini bado kulibakia baadhi itikadi ambazo hazikuweza kuendana sawa na akili, Pia kuna Wanafalsafa wengi Kikristo akiwemo “Thomas Aquinas” waliochukua juhudi kubwa za kufanya marekebisho juu ya itikadi hizo, lakini nao pia hawakuweza kukirekebisha kila kile kilichoonekana kuwa kiko kinyume na akili.
Baada ya kumalizika kipindi cha miaka ya kati na kati, dunia ilionekana kuingia katika zama mpya za kuzaliwa kwa elimu mbali mbali, elimu ambazo zilikuja na mitazo ambayo haikua ikienda sambamba na ile ya Kanisa, mitazamo mbali mbali ya kielimu ambayo ilizaliwa ndani ya zama hizo haikuweza kukubaliana na zile tafsiri zilizokuja kuzisawazisha baadhi ya Itikadi potofu za Kikristo, pia mitazamo ya kielimu iliyokuwa ikitolea na Kanisa haikuwa sawa ile iliyotololewa na wanaelimu mbali mbali wa waliokuja ndani ya zama hizo. Matokeo hayo yaliweza kuzaa msuguano na mgongano uliokuja kuzaa fikra zilizoona kuwa: dini na elimu ni vitu viwili vyenye kupingana, kuenea kwa elimu mbali mbali na kupata nguzvu kwa elimu hizo ndani ya jamii, ndicho kilichosababisha dini ya Kikristo kufifia na kuzima taa yake. Baada ya tokeo hilo wanazuoni wa Kikriso walichukuwa juhudi za hali ya juu ili kukabiliana na tatizo hilo, juhudi ambazo zililenga kuilinda dini yao pamoja na kuzilinda imani za wana jamii wa Wakristo, hapo ndipo walipoamua kuzitangaza maudhui mpya kwa ajili kuitetea dini hiyo. Wanafalsafa wa kidini nao hawakuacha kutoa mchango wao, kwani nao pia walikuja na kuanza kuzichambua maudhui hizo moja baada ya jengine, kitendo ambacho kilizaa sura mpya ya fikra za Kikristo zinazoonekana ndani ya zama zetu za hivi sasa.
Kuna mengi yaliotokea ndani ya historia ya Ukristo tokea mwanzo hadi leo. Ili wasomali wa makala hii waweze kuufahamu uwanja wa kiakili uliowatawala wanachuoni wa Kimagharibi, inatubidi kutoa aina fulani ya ufafanuzi utakaowaongoza wasomaji wetu.
Baada ya wafuasi wa nabii Isa (a.s) kuondokewa na nabii huyu na kupaishwa mbinguni,[1] mitume na wafuasi wake ndiwo waliochukuwa jukumu la kuitangaza dini ya Kikristo katika zama hizo.[2]
Lakini baada ya kupita muda si mrefu alitokea mtu mmoja ajulikanaye kwa jina la “Paul”, naye ndiye mfinyanzi mkuu wa mfumo wa Ukristo uliopo katika zama zetu za hivi sasa, yeye basi alikuja na kukivaa kilemba cha uongozi wa Ukristo ndani ya zama hizo. Paul mwanzoni mwa maisha yake alikuwa ni Myahudi aliyewatesa na kuwaudhi sana Wakristo, na baadae akaingia katika dini ya Kikristo na hatimae akaweza kukubalika vizuri sana mbele ya Wakristo.[3] Yeye alijiweka kama ni mtume (mjumbe) wa Isa (a.s) na akawa anatembea katika vitongoji mbali mbali akiutangaza Ukristo huku akiusongomanisha na kuuposha hatua baada ya hatua.[4]
Dini ya nabii Isa (a.s) haikuwa katika sura mtindo na ulionayo hivi sasa, bali sura hii ya Ukristo inayoonekana katika zama za hivi sasa, inatokana na mfumo wa Paul. Yeye hakuwa na wasiwasi katika kulipoteza neno la Mungu.[5] Miongoni mwa uzushi uliopandikizwa na Paul ndani ya Ukristo, ni Uungu wa Isa, Isa kujitoa muhanga kwa ajili ya makosa ya wengine pamoja na kuifuta sheria ndani ya dini, jambo ambalo alilitowa kutoka kwa washirikina na kuliingiza katika Ukristo.[6] Paul mwishowe alifanikiwa kumgeuza mtume wa Mungu kutoka kwenye cheo cha utume na kumuweka katka kiti cha Uungu, eti Mungu amekuja katika umbile la kibinaadamu ili asulubiwe tendo ambalo liwe ni sababu ya kuwafutia Wakristo dhambi zao!. Hadi leo Wakristo wote wameichukulia imani hiyo kuwa ndiyo msingi mkuu wa dini yao, kiasi ya kwamba iwapo atatokea mmoja wao atakaye amini kinyume na hivyo, basi yeye atakuwa tayari ameshakuwa nje ya dini yake, na atakuwa hana budi kubadili dini yake.
Usambaratishwaji huu wa dini, uliififisha ile ranga ya fikra nzima aliyokuja nayo Isa (a.s), fikra ambayo malengo yake yalikuwa ni kupambana na itikadi potofu zilizojitokeza ndani ja jamii ya Kiyahudi, na wimbi la Paulo (Paul) lililokuja kuzikataa na kuzifunika sheria mbali mbali zenye kuyapa thamani matendo ya wanaadamu,[7] na hilo limekuwa ndiyo sababu kuu iliosababisha dini kuweka katika nafasi ya ushuhuda tu, bila ya dini hiyo kutowa aina yeyote ile ya hukumu maalumu za kuzilinda nafsi za wanaadamu kutokana na dhulma mbali mbali. Ndani ya tamaduni za Kikristo, matendo yenye thamani maalimu ndani ya uwanja wa sheria kama vile (halali na haramu), yamekuwa ni mambo ya kawaida tu yasiyopewa uzito maalumu, kiasi ya kwamba ndani ya Ukristo hakuonekani kuwa kuna matendo ya ulazima yanayomlazimu mtu kuyatenda. Kutokuwa na sheria maalumu si jambo lenye kuonekana ndani ya dini ya Kiyahudi, kwa mfano Wayahudi wanfuata sheria maalumu katika kuchinja vichinjwa vyao, jambo ambalo halionekani ndani ya dini ya Kikristo. Mambo kama haya ndiyo sababu kuu iliosababisha dini ya Kikrito kumeguka kidogo kidogo na kukaa mbali na dini za mbinguni.
Kitabu cha Wakristo [8] nacho hakikukosa nasibu yake katika uwanja wa kuizorotesha dini hii. Matatizo yote ya Ukristo ambayo tumeyataja hapo juu ni ya upande mmoja tu, na upande wa pili kuna tatizo jengine jipya, nalo ni lile tatizo la Injili kukosa mashiko na rejeo maalumu za msingi, wahakiki wa Kimagharibi pia wamelithibitisha jambo hilo.[9] Ukweli ni kwamba kitabu hichi kimeandikwa baada ya kuja Paulo na kuipotosaha dini na baada ya kutokea aina mbali mbali za fitna. Pia Injili hizi ambazo zimo mikononi mwetu, hazionekani kuwa ni zenye sura ya vitabu vya mbinguni, kwani yaliyomo ndani yake ni maneno ya kihistoria tu, yenye kuyazungumzia maisha ya nabii Isa (a.s). Haidhuru ndani ya mazungumzo yake yanayoyazungumzia maisha ya nabii huyo, kuna baadhi ya maneno yanayotokana na Isa mwenyewe (a.s), lakini hilo haliwezi kikifanya kitabu hicho kuwa ni kitabu cha sheria kitokacho mbinguni. Qur-ani inaeleza wazi kuwa nabii Isa (a.s) alishushiwa kitabu chenye sheria na mafunzo maalumu, lakini ni kidogo mno yaliyobakia miongoni mwa mafunzo hayo ndani ya mikono ya Wakristo, na wala hakuna dalili ya kuwepo mabaki ya kitabu hicho ndani ya mikono ya waumini wa dini hiyo.
Ndani ya kipindi cha miaka ya kati na kati (middle ages), wanazuoni wa Kikristo walichukua hatua za kuyarekebisha yale yaliyoonekana kuwa hayaendani na akili miongoni mwa itikadi za Kikristo, na kutaka kuyafasiri katika njia iyendayo sawa na akili, ili kuyapa picha yenye kukubalika kiakili. Mwanafalsafa maarufu wa Kikristo aliyejulikana kwa jina la (Thomas Aquinas) ndiye aliyeibuka kuwa ni shujaa mzuri aliyeweza kutumia akili yake ya Kifalsafa katika kuutetea Ukristo. Thomas Aquinas aliyeishi katika Karne ya kumi na tatu Miladia, alichukua juhudi za hali ya juu kabisa katika kuzirekebisha itikadi za Kikristo. Yeye aliitumia Falsafa ya Kiarosto (Aristotelian Philosophy) ikiwa ni kama nyenzo katika kuitimiza dhamira yake, na kwa kutokana na kuwa yeye alikuwa amezisoma baadhi fikra za Ibnu Sina, pamoja na kuwa na uoni fulani kuhusiana na dini ya Kiislamu, mambo hayo mawili aliweza kuyatumia kuwa ni kama visaidizi katika kuzikarabati fikra za Kikristo, na hatimae yeye aliweza kuleta uhusiano baina ya Falsafa na itikadi za kidini (Kikristo).[10] Jitihada zote zilizochukuliwa na wanavyuoni wa Kikristo, hazikuweza kuleta tiba kamili ya kuzitibu fikra dhaifu za Kikristo zilizoonekana kutoendana na akili. Hadi leo juhudi za Wanafalsafa tofauti wa Kikristo, zimeshindwa kupata tiba halisi ya kulitibu suala la utatu pamoja suala la madai ya Isa (a.s) kuwa ni mtoto wa Mungu, kwani utatu ni wenye kupingana na ile kauli isemayo kuwa Isa (a.s) ni mtoto wa Mungu, kinacholeta mashaka hapa ni kwamba, haiwezekani kuwa Isa (a.s) awe ni mtoto wa Mungu kisha wakati huo huo yeye tena ageuke kuwa Mungu. Haidhuru wao wamejaribu kutafuta suluhu ya tatizo la utatu, tatizo ambalo linaonekana kwenda kinyume na ile itikadi ya Wakristo inayodai kumpwekesha Mungu. Katika kulitatua tatizo hilo wamejaribu kudai kuwa: Mola ni mmoja na ni mwenye tabia moja iliyogawika katika utatu. Utatu huo ni kama ifuatavyo: Baba, Mwana na Roho mtakatifu. Ufumbuzi huu uliotolewa hapa hauwezi kuwa ni suluhu inayokubalika mbele ya mtu mwenye akili timamu.[11] Iwapo Uungu utakuwa ni tabia maalumu iliyogawika katika sehemu tatu tofauti, hii itamaanisha kuwa kuna miungu mitatu yenye sifa na tabia moja, jambo ambalo litakuwa linaukanusha upweke wa Mola Mtakatifu. Si hayo tu yaliyoonekana kuwa ni tatizo kwa wana jamii walioishi ndani ya tawala za Kikristo zilizopita, bali ukirudi nyuma zaidi na kuwaangalia viongozi wa makanisa katika zama kabla ya zama za vumbi la elimu kutibuba, utakuta kuwa kuna mambo mengi yasiokubalika yaliokuwa yakitendeka kupitia mikono ya viongozi hao. Zama ambazo kanisa lilshika nguvu za utawala, zilijulikana kwa jina la (zama za giza) au (Darkness era), zama hizi zikuwa ni kabla ya zama ambazo watu walikuja kupata maendeleo ya kielimu, nazo ni zama zilizojulikana kwa jina la (zama za muamko wa kielimu), ambazo kwa lugha ya Kiingereza zilijulikana kwa jina la (Renaissance era). Katika zama za giza (Darkness era), viongozi wa Kikristo walizishika nafasi muhimu za kisiasa, na moja kati ya masuala muhimu waliyoweza kuwabebesha watu juu ya shingo zao, ni yale madai ya kujidai kuwa wao ni wawakilishi au ni kiungo baina waja na Mola wao, huku wakidai kuwa ni wao tu ndiyo wanaopaswa kushika madaraka katika jamii. Hivyo basi wao waliwalazimisha watu kuwafuata wao katika kila walisemalo. Viongozi wa makanisa ndiwo waliokuwa na jukumu la kuwapangia wengine sheria mbali mbali zilizoegemezwa kwenye mgongo wa dini.[12] Viongozi hao walijaribu kutaka kuziba lile pengo la kuto kuwepo kwa sheria maalumu za kuiongoza jamii ndani ya kitabu chao (Bible), kwa hiyo waliwapangia watu sheria mbali mbali, huku wakidai kuwa ndiyo sheria za kanisa (dini) ili kuziba pengo hilo.
Kanisa katika zama za giza, lilijaribu kuwakalia watu juu ya vichwa vyao, huku likiwanyima wengine ulimi wa kuthibitisha madai yao, kwa hiyo hakukuwa na mtu aliyekuwa na haki ya kutoa elimu bila ya kuwa na ushirikiano wa kanisa, kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa na haki ya kulithibitisha jambo bila ya kupata muhuri wa kanisa (ruhusa).
Baada ya watu kuwa tayari wameshachoshwa na hali hiyo, hapo ndipo zilipokuja zama za kutibuka kwa vumbi la elimu mbali mbali za Kifalsafa na Kisayansi. Viongozi wa kanisa walijaribu kuisongomanisha ile mitazamo mbali mbali ya kielimu na kuifasiri watakavyo wao kwa ajili ya manufaa ya kanisa, jambo ambalo lilisababisha kuzaliwa fikra mpya isemayo kuwa: dini ni yenye kwenda kinyume na mitazamo sahihi ya kielimu. Fikra hizo zilizoona kuwa dini na elimu ni vitu viwili tofauti vyenye kusuguana, na mtazamo huo ndiwo ulioisababisha taa ya Ukristo (kanisa) kufifia siku baada ya siku. Baada ya tokeo hilo, wanazouoni na Wanafalsafa mbali mbali wa kanisa, walijaribu kuibuka na fikra mbali mbali zenye sura mpya ya kuutetea Ukristo. Na hiyo ndiyo hali halisi ya maisha ya dini ya Kikristo yalivyokuwa tangu mwanzo hadi leo. Hivyo basi hutoacha wewe kuwaona Wanfalsafa mbali mbali wa Kikristo wanaopiga maji kwa ajili ya kutaka kuiokoa dini yao.
Kwa ufafanuzi zaidi rejea kitabu:
1- Wilaayat wa diyaanat, cha Ayatullahi Mahdi Hadawiy Tehraniy, chapa ya Muaseseye farhangiy khoneye kitab, Qum Iran, chapa ya pili ya mwaka 1380 Shamsia.
2- Mabani kalamiy jadid ijtihadi, cha Ayatullahi Mahdi Hadawiy Tehraniy, chapa ya kwanza ya Muaseseye farhangiy khoneye kitab, Qum Iran, 1377 Shamsia.
[1] Kwa mtazamo wa Kiislamu na Qur-ani, nabii Isa (a.s) hakusulubiwa bali alipaishwa na Mola wake mbinguni. Lakini Wakristo wanaamini kuwa alisulubiwa kisha akazikwa, na baada ya hapo akafufuka, na kwa kipindi cha siku 40 au 30 alikua akija kwa wafuasi wake na kuwatembelea, kisha baadae akapaa mbinguni. Rejea Qur-ani, Aya ya 157-158. Injili ya Luka katika mlango wa 24. Agano jipya kitabu cha Matendo ya mitume mlango wa kwanza.
[2] Agano jipya mlango wa Matendo ya mitume.
[3] Kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi kuhusianan na imani ya Paul, rejea Agano jipya/kurasa zinazozungumzia Matendo ya mitume/ kuanzia mlango wa tisa na kuendelea.
[4] Ndani ya rejeo za Hadithi mbali mbali ndani ya dini ya Kiislamu, Paul ameweka daraja moja na watu kama vile: Firauna na Namrudh, naye ni miongoni mwa watu watakaopata moto ulio mkali zaidi. Rejea Biharul-anwaar, uk/311, juz/8.
[5] Hamphrey Carpenter, Isa, uk/154.
[6] Baadhi wahakiki wa Kimagharibi wamelielezea suala hilo kwa marefu. Rejea kitabu cha historia za dini cha John B. NAS, uk/617. Agano jipya, barua (risala) ya Paulo kwa Wagalatia na barua ya kwanza ya Paulo kwa Wakorintho, barua ya kwanza kwa Timotheo pia rejea Humphrey Carpenter, Isa, uk/154.
[7] Sheria ni sehemu maalumu ya dini inayofungamana na matendo ya mwanaadamu mbele ya Mola wake, mbele ya wanajamii na mbele ya viumbe vyengine. Na aina hii ya sheria inajulikana kwa jina la (fiqhi).
[8] Bible.
[9] Inadaiwa kuwa mapokezi ya Injili hii ni yenye kushikana mkono kwa mkono hadi kufikia miaka miaka mia mbili baada ya kufa Kristo. Rejea (ulimwengu wa kidini cha Robert Weir, juz/2 uk/675. Hamphrey Carpenter, Isa, uk/12-32.
[10] Rejea kitabu comprehensive history of religions cha John B. NAS, uk/658-660. Pia kitabu Religious world cha Robert Weir, juz/2, uk/733-734.
[11] Rejea kitabu Religious world cha Robert Weir, juz/2, uk/134-138.
[12] Cannon law.